Deuteronomy 5:1-21

Amri Kumi

(Kutoka 20:1-17)

1 aMose akawaita Israeli wote, akawaambia:

Ee Israeli, sikilizeni amri na sheria ninazowatangazia leo. Jifunzeni, na mwe na hakika kuzifuata.
2 bBwana Mungu wetu alifanya Agano nasi katika mlima wa Horebu. 3 cSi kwamba Bwana alifanya Agano na baba zetu, bali alifanya nasi, nasi sote ambao tuko hai hapa leo. 4 dBwana alisema nanyi uso kwa uso kutoka moto juu ya mlima. 5 e(Wakati huo nilisimama kati ya Bwana na ninyi kuwatangazia neno la Bwana, kwa sababu mliogopa ule moto, nanyi hamkupanda mlimani.) Naye Mungu alisema:

6 f“Mimi ndimi Bwana Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.

7 g“Usiwe na miungu mingine ila mimi.
8 hUsijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni au duniani chini au ndani ya maji. 9 iUsivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, 10 jlakini ninaonyesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanipendao na kuzishika amri zangu.
11 kUsilitaje bure jina la Bwana Mungu wako, kwa kuwa Bwana hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure.
12 lAdhimisha siku ya Sabato na kuiweka takatifu, kama Bwana Mungu wako alivyokuagiza. 13Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote. 14 mLakini siku ya Saba ni Sabato kwa Bwana, Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wa kiume au mtumishi wa kike, wala ngʼombe wako, punda wako au mnyama wako yeyote, wala mgeni aliyeko malangoni mwako, ili kwamba mtumishi wako wa kiume na wa kike wapate kupumzika kama wewe. 15 nKumbuka mlikuwa watumwa huko Misri, na Bwana Mungu wenu aliwatoa huko kwa mkono wenye nguvu na kwa mkono ulionyooshwa. Kwa hiyo Bwana Mungu wako amekuagiza kuiadhimisha siku ya Sabato.
16 oWaheshimu baba yako na mama yako, kama Bwana Mungu wako alivyokuagiza, ili siku zako zipate kuwa nyingi na kufanikiwa katika nchi Bwana Mungu wako anayokupa.
17 pUsiue.
18 qUsizini.
19 rUsiibe.
20 sUsimshuhudie jirani yako uongo.
21 tUsitamani mke wa jirani yako. Usitamani nyumba ya jirani yako au shamba lake, mtumishi wake wa kiume au wa kike, ngʼombe au punda wake, wala kitu chochote cha jirani yako.”
Copyright information for SwhNEN